Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza A‘rafi, Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu, katika Kongamano la Kitaifa la Fiqhi na Maadili lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Qur’ani na Hadith, alichambua uhusiano kati ya fiqhi na maadili na akasisitiza umuhimu wa kuutazama upya uhusiano huo.
Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu mwanzoni alirejea maadhimisho ya miaka elfu moja na mia tano tangu kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w), pamoja na wito wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi wa kuimarisha mazoea ya kushikamana na Nahjul Balagha, kisha akanukuu sehemu ya Hotuba ya 94 ya Nahjul Balagha katika kumuelezea Mtume Mtukufu (s.a.w.w).
Ayatullah A‘rafi aliendelea kwa kuchambua uhusiano kati ya fiqhi na maadili, akasema: Inawezekana mtu akaona elimu ya kalamu (itikadi) na fiqhi kuwa ni nyanja mbili zilizo tofauti kabisa, lakini akasema kwamba hizi mbili kwa pamoja ni kama mabawa mawili ya mfumo mmoja. Sifa za kimaadili zinaweza kuwa mada ya hukumu za kifiqhi, na “fiqhi lazima iweze kushughulikia vipengele mbalimbali vya kibinadamu na kimaadili.”
Hotuba Kamili ya Ayatullah Alireza A‘rafi katika Kongamano la Kitaifa la Fiqhi na Maadili ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Ni maadhimisho ya miaka elfu moja na mia tano tangu kuzaliwa Mtume Mtukufu, na pia kuna wito wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi wa kuimarisha mazoea ya kushikamana zaidi na Nahjul Balagha. Pia nitataja kifungu kutoka katika Nahjul Balagha kuhusiana na Mtume (s.a.w.w) katika mkesha wa Bi‘tha tukufu. Katika Hotuba ya tisini na nne, hii ni mojawapo ya takriban sehemu ya arobaini au hamsini kwenye Nahjul Balagha ambapo Amir wa ufasaha Imam Ali (a.s) amezungumza kuhusu taswira ya Mtume:
«عِتْرَتُهُ خَیْرُ اَلْعِتَرِ وَ أُسْرَتُهُ خَیْرُ اَلْأُسَرِ وَشَجَرَتُهُ خَیْرُ اَلشَّجَرِ نَبَتَتْ فِی حَرَمٍ وَبَسَقَتْ فِی کَرَمٍ لَهَا فُرُوعٌ طِوَالٌ وَ ثَمَرٌ لاَ یُنَالُ فَهُوَ إِمَامُ مَنِ اِتَّقَی وَبَصِیرَةُ مَنِ اِهْتَدَی سِرَاجٌ لَمَعَ ضَوْؤُهُ وَشِهَابٌ سَطَعَ نُورُهُ وَزَنْدٌ بَرَقَ لَمْعُهُ سِیرَتُهُ اَلْقَصْدُ وَسُنَّتُهُ اَلرُّشْدُ وَکَلاَمُهُ اَلْفَصْلُ وَ حُکْمُهُ اَلْعَدْلُ و...»
“Kizazi chake ni bora kuliko vizazi vyote, familia yake ni bora kuliko familia zote, mti wake ni bora kuliko miti yote; umeota katika Haram na umekua katika ukarimu; una matawi marefu na matunda yasiyofikiwa. Yeye ni kiongozi wa wachamungu, ni nuru ya waongofu, ni taa inayong’aa mwanga wake, ni kimondo chenye nuru inayong’aa, ni cheche inayomeremeta. Mwenendo wake ni wa kati, sunna yake ni uongofu, maneno yake ni yenye kutenganisha haki na batili, na hukumu yake ni uadilifu …”
Huyu alikuwa jua linalong’aa na taa yenye nuru, ambalo kwa Bi‘tha yake liliuangazia ulimwengu na kuuangazia hadi Siku ya Kiyama kwa nuru za maarifa na maadili.
Tunawashukuru waandaaji wa kongamano na wote waliotoa hoja na maoni katika mada hii muhimu. Nitataja kwanza hoja mbili, kisha nitachagua machache miongoni mwa hoja nyingi nilizoandika na kuziwasilisha mbele yenu.
Hoja ya kwanza ni kwamba tofauti au umoja kati ya fiqhi na maadili ni suala linalohitaji tafakuri. Hoja ya pili ni kwamba elimu mbalimbali zinaweza kuwa na malengo na makusudio yanayofanana, au zikaunda mfumo mmoja ulioungana kwa ajili ya sa‘ada (ustawi) ya mwanadamu. Inawezekana mtu akaona elimu ya kalamu na fiqhi kuwa ni tofauti kabisa, lakini akasema kuwa kwa pamoja ni mabawa yanayounda mfumo mmoja. Hili pia ni kweli ndani ya elimu moja.
Kwa mujibu wa mgawanyo wa marehemu Muhaqqiq, fiqhi imegawanywa katika sehemu nne, kila moja ikiwa na sifa zake lakini zote zikiwa ndani ya mfumo mmoja wa jumla. Huu ni mpangilio wetu.
Marehemu Ayatullah Misbah (r.a) alieleza vizuri katika uchambuzi wake wa mwisho kwamba utengano wa elimu, wakati mwingine ni wa kihakika na wakati mwingine ni wa kimkataba. Kwa mfano, kutenganisha saikolojia ya ukuaji na saikolojia ya kijamii ni mgawanyo wa kimkataba. Kwa hakika, katika saikolojia ya ukuaji tunachunguza upande mmoja wa nafsi ya binadamu, na katika saikolojia ya kijamii tunachunguza upande mwingine. Utengano huu umetokana na kuongezeka kwa masuala na mada.
Katika misingi ya elimu, mjadala mkubwa umefanyika kuhusu utofautishaji wa elimu, na mojawapo ya nadharia mashuhuri ni kwamba utofautishaji wa elimu upo kwa maana ya kihakika, kwa kuwa kila elimu hushughulikia sehemu maalumu ya uhalisia, na pia upo kwa maana ya kimkataba, kwa kuwa mgawanyo huu umeundwa kwa misingi ya mahitaji na maendeleo ya elimu.
Kwa sababu mada nyingi katika ulimwengu wa uhalisia zimeungana, tunaweza wakati mwingine kuunganisha nyanja tofauti za mada moja na kuunda dhana pana zaidi, au tunaweza kuzitenganisha. Mageuzi haya pia yamekuwepo katika historia ya elimu. Kwa mfano, "ta‘lim na tarbiya" hapo awali haikutambuliwa kama elimu, bali kama ujuzi wa vitendo. Baadaye, kutokana na maendeleo ya elimu, ikawa taaluma ya kielimu yenye matawi mbalimbali.
Kwa hiyo, kwa mtazamo mmoja kuna umoja na utofauti wa kihakika, lakini kwa mtazamo mwingine, mtazamo wetu wa kidhihinia hatupaswi kuwa na wasiwasi mkubwa juu ya utofauti huu, mtu anaweza kusema kwamba maadili ni sehemu ya fiqhi, au anaweza kusema kwamba kwa sababu ya sifa zake maalumu, imekuwa elimu huru, lakini uwepo wa umoja na mgawanyiko haupingani na mfumo mmoja wenye malengo yaliyo wazi na ya pamoja.
Hoja ya Pili: Nadharia Kuhusu Uhusiano wa Fiqhi na Maadili
Kwa mtazamo wa jumla, kuna nadharia tatu kuu:
1. Nadharia ya kwanza: Fiqhi na maadili ni eleimu mbili zisizo na mafungamano kabisa, mada na hukumu zake ni tofauti kabisa.
2. Nadharia ya pili: Kiasili fiqhi na maadili ni kitu kimoja, na mgawanyiko uliopo umetokana na historia ya maendeleo ya maadili nje ya mazingira ya sheria.
3. Nadharia ya tatu: Mtazamo wa kati unaosema kuwa kila upande una kiini chake huru, lakini kuna maeneo mengi ya pamoja yanayopaswa kushughulikiwa kifiqhi.
Ninaamini nadharia ya tatu ina uzito zaidi. Kuna mahusiano hata katika viini muhimu vya pande zote mbili. Ikiwa tutasema kiini cha maadili ni kuchunguza sifa njema na mbaya, namna ya kupata, mahusiano yake na athari zake katika nafsi, basi haya yote yana uhusiano wa karibu na fiqhi.
Hata kama tutasema baadhi ya masuala haya hayaingii katika maadili kwa maana mahsusi, bado yana athari na lazima yaakisiwe katika fiqhi. Hii inaandaa njia ya kukubali kuwa kuna viini tofauti katika fiqhi na maadili, lakini pia kuna miduara mingi ya pamoja.
Kwa mtazamo huu mpana wa fiqhi, tunaweza kusema kuwa hukumu tano za kifiqhi (wajibu, haramu, mustahabu, makruhu na halali) zote ni sehemu ya fiqhi. Dai la kwamba mustahabu au makruhu havimo katika fiqhi si sahihi. Viwango vya hukumu vinaonesha kiwango cha umuhimu na uangalizi.
Kwa mtazamo huu, masuala mengi ya kimaadili yanaweza kuingia katika fiqhi na kupangiwa hukumu za kifiqhi. Vivyo hivyo, vitendo vya ndani vya mwanadamu, pale vinapokuwa vya hiari, vinaweza kuwa mada ya fiqhi.
Fiqhi ya itikadi ipo, na hukumu za kiimani pia zina wajibu, uharamu, au istihbabu, kwa sababu imani inaweza kupatikana kupitia utangulizi wa hiari. Hivyo, mlango wa “Fiqhi ya Itikadi” unahitajika.
Kadhalika, fiqhi ya mahusiano ya kijamii, fiqhi ya maadili ya kijamii, na fiqhi ya hali za ndani za nafsi zote zinahitaji kupangiliwa katika mfumo wa kifiqhi.
Kwa mtazamo huu, karibu masuala yote ya kalamu na maadili yanaweza kuwa na mtazamo wa kifiqhi, jambo linalofungua milango mipya ya maendeleo ya fiqhi. Lengo la fiqhi si tu thawabu au kuepuka adhabu, bali pia shukrani kwa Mwenyezi Mungu, upendo wa Mwenyezi Mungu, na hatimaye utiifu kamili na kufikia katika uzuri na utukufu Wake.
Kwa hiyo, ingawa malengo yanaweza kutofautiana kwa viwango, hakuna mgawanyiko wa kimsingi kati ya malengo ya fiqhi na maadili.
Maoni yako